KIKAO CHA KUPOKEA RIPOTI YA UTAFITI WA SOKO LA AJIRA KWA WAHITIMU WA MAFUNZO YA VYUO VYA AMALI ZANZIBAR

Kamishna wa Kazi – Kamisheni ya Kazi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi Ndugu Rashid Khamis Othman amesema Utafiti wa Soko la Ajira utasaidia katika kutatua changamoto za ajira zilizopo nchini.

Kamishna Rashid ameyasema hayo kwa Niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji wakati wa kikao cha kupokea Ripoti ya Utafiti wa Soko la Ajira kwa Wahitimu wa Mafunzo ya Vyuo vya Amali Zanzibar huko katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi.

Amesema soko la ajira linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ajira kwa vijana, kukosekana kwa vijana wenye ujuzi na ushawishi mdogo wa teknolojia na ubunifu.

Amesema, utafiti huo utaenda kusaidia kupata takwimu sahihi za vijana waliopo katika soko la ajira pamoja na kuweza kuisaidia Serikali katika kupanga mikakati imara kwa vijana hao.

Nae, Meneja wa Mradi wa Kuwajengea Uwezo Vijana Kujiajiri na Kuajirika Kupitia Uchumi wa Bluu (SEBEP) Ndugu Said Mkubwa Abdallah amesema mradi huo unaenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar mwaka 2050 ambao upo chini ya Wizara ya Elimu na unadhanimiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika wenye lengo la kuwajengea uwezo vijana hasa katika sekta ya uchumi wa bluu.

Akiwasilisha Ripoti ya Utafiti huo Profesa Deograsias Mushi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salam amesema uliowashirikisha waajiri, wahitimu wa Vyuo na Taasisi za Serikali na Binafsi wenye lengo la kuangalia namna fursa za ajira zilizopo katika soko za ajira zinavoendana na wahitimu wa Vyuo vya Mafunzo ya Amali Zanzibar hasa katika Sekta ya Uchumi wa Buluu.

Amesema, matokeo ya utafiti huo umeonesha kuwa baadhi ya ujuzi unaotolewa na Vyuo vya Mafunzo ya Amali hauendani na soko la ajira liliopo, ukosefu wa vifaa, kuwepo vifaa visivyokidhi na teknolojia iliyopo, kutokukidhi sifa kwa baadhi ya walimu wa vyuo hivyo pamoja na ushiriki mdogo wa wanawake.

Kikao hicho cha siku moja kimefungwa na Afisa Mdhamini Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Dkt. Fadhila Hassan Abdallah.