MAKABIDHIANO YA IDARA BAINA YA WIZARA YA KAZI NA UWEKEZAJI NA WIZARA YA VIJANA AJIRA NA UWEZESHAJI

MABADILIKO YA WIZARA HAYAKUFANYIKA KWA BAHATI MBAYA – WAZIRI SHARIFF
************
Waziri wa Kazi na Uwekezaji Mheshimiwa Shariff Ali Shariff ameziomba Idara ya Ajira, Idara ya Maendeleo ya Ushirika na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuongeza bidii katika kusimamia masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuweza kutimiza malengo ya Serikali ya kuzifikia ajira Laki Tatu na Hamsini.

Hayo ameyaeleza katika makabidhiano ya Idara baina ya Wizara ya Kazi na Uwekezaji na Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji huko Ofisini Mwanakwerekwe.

Amesema kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi hayakuwa ya bahati mbaya bali ni njia sahihi ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji.

Amesema kuwa, kupitia Idara ya Maendeleo ya Ushirika na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi zilifanya kazi kubwa katika kuwasaidia wananchi ambapo kiasi cha shilling Bilioni Tisiini na Sita zilifanikiwa kutolewa kwa wananchi ikiwemo makundi maalumu ili kuwainuwa kiuchumi kupitia shaghuli zao mbali mbali za ujasiriamali wanazozifanya.

Aidha, ameongezea kuwa kupitia Idara ya Ajira imefanikiwa kuimarisha upatikanaji wa ajira za staha za ndani na nje ya nchi jambo ambalo limesaidia wananchi kujikwamuwa na umasikini pamoja na kuongeza pato la Taifa.

Amefahamisha kuwa, katika taasisi na Idara hizo wapo wataalamu wa kutosha wenye bidi na uwadilifu katika kusimamia majukumu yao ya kazi, hivyo amewasisitiza watendaji hao kuwapa mashirikiano viongozi walioteuliwaili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Hata hivyo, Mheshimiwa Shariff amewashauri viongozi wa Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji kupitia tena Sheria, Sera, Kanuni na Miongozo iliyopo awali ili kubaini maeneo yanayohitaji kufanyiwa marekebisho ili ziweze kuendana na kasi ya utekelezaji ya majukumu na mahitaji ya sasa ya kiutendaji.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano ya Idara hizo Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji Mheshimiwa Shaaban Ali Othman amesema Wizara hiyo bado inahitaji mashirikiano ya dhati kutoka Wizara ya Kazi na Uwekezaji ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo.

Waziri Shaaban ameahidi kutekeleza majukumu kwa kuzingatia kasi ya Serikali ya Awamu ya Nane ili kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma zilizobora na kwa wakati.