IDARA YA USALAMA NA AFYA KAZINI YAWAPIGA MSASA WADAU WA UTATU
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Ndugu Khamis Suleiman Mwalim amezitaka Taasisi za Serikali na Binafsi zilizopo nchini kuitumia Idara ya Usalama na Afya Kazini kwa ajili ya kufanyiwa usajili ili waweze kukaguliwa na
kuweza kufanya kazi katika mazingira salama .
Ameyazungumza hayo wakati akifungua mkutano wa kuwapa uelewa wadau wa usalama na afya kazini huko Ofisini Mwanakwerekwe.
Amesema, kufanya hivyo kutasaidia Taasisi hizo kujikinga na majanga na ajali zinazoweza kujitokeza katika sehemu za kazi.
Amesema, ni vyema kwa waajiri kufuata ushauri wa kitaalamu na maelekezo yanayotolewa na idara hiyo juu ya utekelezaji bora wa kazi zao.
Aidha, amewasisitiza waajiri kuwafanyia uchunguzi wa afya wafanyakazi wao wakati wanapoajiriwa, wanapoendelea na majukumu yao ya kazi na baada ya kustaafu kazi ili kuweza kujua athari za kiafya walizonazo.
Wakiwasilisha Mada ya Dhana ya Idara ya Usalama wa Afya Kazini Zanzibar Ndugu Ame Faki Saleh pamoja na Meneja wa Usalama wa Afya Kazini kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Mhandisi Robert Mashinji wamesema ni vyema kwa Taasisi na Makampuni kuwa na ushirikiano wa pamoja na idara hizo ili kuweza kurahisisha kazi zao na kusaidia kuondoa changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa kazi zao.
Nao Washiriki wa kikao hicho akiwemo Ndugu Hassan Ali Ngozi amesema Idara ya Usalama imepata mabadiliko makubwa baada ya kuingia Serikali ya awamu ya nane kwa kuweka msisitizo katika masuala ya usalama na afya kazini pamoja na kuishauri Idara hiyo kuendelea kutoa taaluma na ushauri kwa waajiri na wafanyakazi.




